MAISHA YA CHUONI, TAMATI NIMEFIKA

 Kumbukizi za kujiunga na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa almaarufu Technical University of Mombasa,bado zimo akilini mwangu.Siku hiyo ya kujiunga na Chuo hiki ilikuwa Jumatatu ya tarehe ishirini na tano ya mwezi Januari mwaka wa elfu mbili ishirini na moja masaa ya asubuhi.Hapo awali nilikuwa nimepata mwaliko wa kujiunga na Chuo hiki kusomea taaluma ya habari na Mawasiliano.Ni ndoto ambayo nilitamani Sana siku moja kuwa mwanahabri tajika kama Rashid Abdhalah wa runinga ya Citizen.Siku hiyo nilivalia suti ya rangi nyeusi tititi na shati leupe pepepe kama maziwa huku likiwa limepigwa pasi kiasi ya kwamba nzi angetua juu ya shati hilo basi angefariki papo hapo.

Nilifika katika afisi za usajili wa wawanagenzi,nikakabidhiwa barua ya usajili kisha nikaamuriwa kujaza nafasi zilizoachwa wazi.Kwa kuwa ilikuwa siku yangu ya kwanza kukanyaga chuo hicho,sikuwa na budi ila kuomba msaada wa kuelekezwa jinsi ya kujaza fomu hiyo.Kulitokea janadume ila lilinipea masharti ambayo sikuweza kuyaepuka Kwa maana nilihitaji msaada wake Kwa asilimia kubwa.Mwanaume huyo alinielekeza jinsi ya kujaza fomu hiyo kisha baadae nikampatia hela kidogo kama alivyoniamuru hapo awali.

Mwaka wangu wa kwanza nliona kama mateso lakini baadae nilikujamaizi kuwa maji ukiyavulia nguo ni sharti kama ibada uyaoge.Kusema kweli ni kwamba,safari yangu ya maisha ya chuoni, imekuwa ya panda shuka, milima na mabonde.Walumbi wa lugha walisema Sheria ni kama msumeno hukata mbele na nyuma ila kwangu nilizifuata kisawasawa kama sala za siku hadi sasa tamati nikielekea.Nimekuwa Mwanafunzi mtiifu,mwaminifu,mkarimu ,mpole sikwambii mcheshi, sifa sufufu zinazidi kumiminika kwangu mithili ya mvua huku masomo yangu yakielekea ukingoni.

Ni mengi nimepitia ,zikiwemo dhiki chungu nzima.Kwanza kabisa,Karo ya shule ndilo donda sugu lililonikodolea macho tangia mwanzo wa masomo.Basari na misaada kutoka Kwa wahisani wema ndio imekuwa hewa nayopumua.Sina la kuwalipa waja wote wanaoendelea kufanikisha ndoto yangu ya uanahabari ila nawaombea Jaala Jalia awajalie na kuwajazia pahali popote pale palipopungua.Fauka ya hayo,maisha ya chuo Kikuu yamenisaidia katika kujuana na watu tofauti tofauti kutoka pembe zote za taifa letu tukufu la Kenya.Nimejenga urafiki,nimejifunza lugha tofauti tofauti,nimeiga tabia na mienendo tofauti ya makabila yote ya Kenya.

Sasa ni tabasamu limejaa usoni mwangu huku nikijuwa fika kuwa muda kiduchu ndio uliosalia kueka kikomo sentensi ya masomo ya chuo Kikuu.Ifikapo tarehe ishirini na tatu ya mwezi Disemba mwaka huu, majengo ya chuo kikuu cha Kiufundi cha Mombasa nitayaona paa. 

Wanasema kilicho na mwanzo hakikosi mwisho,shukrani za dhati kwa Allah Kwa kuniwezesha kudurusu toka chekechea hadi hatua hii,pia familia yangu kwa mpigo naipa kongole kwa kunipea nafasi mahususi ya kipekee ya kunipeleka shuleni.Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa, wanagenzi wenza walioshirikiana nami katika somo hili la mtandaoni, pamoja na washikadau wote bila kuwasahau wahisani  waliohusika katika masomo yangu sitowaacha nyuma kamwe , Maulana awabariki popote mlipo.Nitazidi kuwatilia dua Kwa Rabana muumba wa ardhi na mbingu atuzidishie neema na rehema pamoja na siha njema.Masalam!


Mwandishi wa makala haya ni;

Mohammed Kazungu (Mwanahabari mtarajiwa)

Kutoka Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM)


Comments

  1. Tunamrudishia maulana shukrani kwa kutuezesha 🙏

    ReplyDelete
  2. Wow🥰 In love with the article

    ReplyDelete
  3. Umekuwa muda mfupi ila wenye faida kiujumla. kazi safi

    ReplyDelete
  4. Hongera sana mwanahabari mtarajiwa.
    Kazi safi

    ReplyDelete
  5. Hongera sana Kwa kazi safi uzidi kung'ara siku za usoni 👏

    ReplyDelete
  6. Kazi mbashara, hongera Allah akujaalie njozi yako itimie inshallah

    ReplyDelete
  7. Ukweli kabisa kaka,hongera👏👏👏

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

HALUWA SI TAMU TENA VYUONI

MALEZI

BAADA YA DHIKI FARAJA